WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Saturday, 15 July 2017

Masauni aliagiza Jeshi la Polisi kufungua kituo makazi ya kabila la Wahazabe



Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Polisi mkoani Manyara kufungua Kituo cha Polisi katika Makazi ya Kabila la Wahazabe wanaoishi katika Bonde la Yueda Chini, wilayani Mbulu.

Masauni alisema hayo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kabila  hilo mara baada ya kukagua jengo la mifugo katika eneo la bonde hilo ambalo jamii hiyo ilijitenga kwa kuweka makazi pembezoni mwa Mji wa Mbulu.

“Hivi karibuni Kituo cha Polisi kitafunguliwa hapa ili kulinda usalama wenu katika eneo hili ambalo lilikua halina kituo cha Polisi kwa miaka mingi. Serikali ya Rais Magufuli ni sikivu ndio mana nimekuja hapa kuwasikiliza matatizo yenu na kuwatekelezea.” Alisema Masauni huku akishangiliwa na wananchi hao.

Aliongeza kuwa, mchakato wa kujenga kituo hicho umeanza na tayari ametoa maelekezo kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa huo, kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Wabunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini na Mbulu Mjini.

Pia aliongeza kuwa, uhalifu katika eneo hilo sasa umepata tiba kwa maana Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi watahakikisha hali ya usalama unaimarishwa zaidi katika eneo hilo ambalo lipo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay alisema wananchi wa jimbo lake wanavamiwa, wanaporwa mali zao ikiwemo mifugo, wanajeruhiwa na wanaingizwa katika umaskini zaidi kutokana na waalifu kuwa wengi kutokana na ukosefu wa Kituo cha Polisi.

“Nilimuomba na nilimsumbua sana Naibu Waziri kule Bungeni ili aweze kufika katika eneo hili, ninamshukuru sana kwa kufika na kutoa maelekezo ya kufunguliwa kituo cha polisi, sasa wakazi wa eneo hili tunatarajia kupata ulinzi wa kutosha baada ya kituo hicho kufunguliwa hivi karibuni,”alisema Massay.

Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Francis Massawe alisema amepokea maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri na mchakato utaanza rasmi na hatimaye kituo cha Polisi kitakuwepo katika eneo hilo na wananchi wataendelea na shughuli zako za kutafuta mahitaji yao kwa usalama zaidi.

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

MASAUNI AWATAKA MAAFISA UHAMIAJI, POLISI KUONGEZA KASI KUCHUNGUZA NA KUWAKAMATA WAHAMIAJI HARAMU TANGA

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akimfafanulia jambo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela (kulia) kabla ya kiongozi huyo kuanza ziara yake mkoani humo. Katika mazungumzo yao ambayo yalifanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huyo, Masauni aliwataka maafisa uhamiaji pamoja na Polisi kuongeza kasi ya kutafuta mizizi ya wahamiaji haramu mkoani humo. Kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Benedict Wakulyamba.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (watatu kushoto) akimsikiliza  Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela (katikati) alipokua anatoa taarifa ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, kabla ya kiongozi huyo kuanza ziara yake mkoani humo. Katika mazungumzo yao, Masauni aliwataka Maafisa Uhamiaji pamoja na Polisi kuongeza kasi ya kutafuta mizizi ya wahamiaji haramu mkoani humo. Kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Benedict Wakuliamba.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto) akitoka kulikagua jengo la Ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tanga ambalo linahitaji matengenezo ili kulirudisha katika hali yake ya kawaida. Hata hivyo, Masauni alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba (kulia) kuhakikisha jengo hilo linatengenezwa haraka iwezekavyo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia) akizungumza na Viongozi wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara yake, mkoani Tanga wakati kiongozi huyo alipofanya ziara yake kikazi mkoani humo. Katika mazungumzo yao, Masauni aliwahasa viongozi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa kujituma zaidi na kuwahakikishia kero zote walizompa atahakikisha anazifanyia kazi. Kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Benedict Wakulyamba. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni  (kushoto) akimfafanulia jambo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela (katikati) na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Zena Saidi, kabla ya kiongozi huyo kuanza ziara yake mkoani humo. Katika mazungumzo yao ambayo yalifanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huyo, Masauni aliwataka maafisa uhamiaji pamoja na Polisi kuongeza kasi ya kutafuta mizizi ya wahamiaji haramu mkoani humo. Picha  na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.