WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Friday 18 March 2016

KITWANGA ATEMBEA MITAANI AKICHUKUA MAONI YA WANANCHI PEMBA, WANANCHI WASEMA HAKUNA VURUGU, WANAENDELEA NA SHUGHULI ZAO KAMA KAWAIDA

Na Mwandishi Wetu, MOHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka wananchi wa Zanzibar waondoe hofu kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu visiwani humo.
Akizungumza mara baada ya kufanya mazungumzo na wananchi hao wakati alipokuwa anatembelea mitaa mbalimbali ya Soko Kuu la mjini Chake Chake, Pemba aliwataka wananchi hao waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato kama kawaida na hakuna mtu atakayewabughudhi kwani ulinzi umeimarishwa, na waachane na uzushi wa kutokea vurugu unaoenezwa visiwani humo.
Waziri Kitwanga alianza matembezi hayo mitaani mara baada ya kufanya mazungumzo na Kamati ya Ulinzi na Usalama mjini Chake Chake ambapo walimuhakikishia kuwa, Pemba yote ni salama na ulinzi umeimarishwa na hakuna atakaye fanyiwa vurugu kwa mtu yeyote atakayefuata sheria.
Waziri Kitwanga aliwataka wananchi hao kuondoa hofu wanapowaona askari mbalimbali wakipita mitaani kwani wapo kwa ajili ya kuwalinda wananchi hao pamoja na mali zao katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.
“Musiwaogope askari, na wala msiwe na wasiwasi, mnapowaona shangilieni kwani askari ndio msaada wako kwa ajili ya usalama wako endapo inapotokea vurugu ya aina yoyote, mtaenda kupiga kura salama na mtarudi salama, hakuna mtu wa kuwabughudhi, msitishwe na mtu yeyote,” alisema Waziri Kitwanga na kufafanua;
“Leo nazunguka mitaa mbalimbali ya hapa Pemba, lengo ni  kuchukua maoni yenu pamoja na kuwaondolea hofu wananchi na kuwahakikishia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimejipanga vizuri kwa ajili ya kulinda usalama, hivyo jitokezeni kwa wingi siku ya uchaguzi mkapigie kura kiongozi mnaemtaka.”
Hata hivyo, Waziri Kitwanga alifanya ziara Mkoa wa Kaskazini Pemba katika msitu wa Ngezi unaodaiwa kuwa kuna baadhi ya wakimbizi wamejificha katika msitu huo ili kuokoa maisha yao baada ya kudaiwa kuwa kutatokea na vurugu.
Kitwanga akiongozana na Wakuu wa Mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba pamoja na maafisa wa Jeshi la Polisi Pemba, walienda katika msitu huo na kuukagua na hawakukutana na mtu hata mmoja aliyejificha msituni humo kama inavyodaiwa na kusambazwa habari na baadhi ya watu wasioitakia mema Zanzibar.
“Ndugu waandishi wa habari, tumezunguka kwa pamoja kuungalia msitu huu, kuwatafuta hao wakimbizi, hatujamuona mtu yeyote, ukisikia propaganda ndio hii, watu hawaitakii mema Zanzibar na Tanzania kiujumla, mmeona kuwa habari hii ni ya uongo, hakuna mkimbizi yeyote katika msitu huu kama tulivyoshuhudia wote kwa ujumla,” alisema Kiwanga.
Aliongeza kuwa, baadhi ya wananchi ambao wana mipango yao binafsi wanawatia hofu wananchi kwa kutunga habari za uongo kuwa Zanzibar imechafuka, wakati habari hizo hazina uhalisia wowote.
Hata hivyo, wananchi wa Pemba walimuhakikishia Waziri Kitwanga wanafanya shughuli zao za kuwapatia kipato kama kawaida na pia siku ya uchaguzi wataenda kupiga kura kama kawaida kwani wanaamini amani itakuwepo kama ilivyokuwa sasa.
Waziri Kitwanga alifanya ziara Zanzibar katika Kisiwa cha Unguja na kuzungumza na Maafisa wa Jeshi la Polisi na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, na baadae kumalizia ziara yake kwa kutembelea katika mikoa yote ya Pemba ikiwa ni hatua ya kuangalia hali ya usalama visiwani humo katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu katika maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment