WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka wananchi wa Zanzibar
waondoe hofu kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu visiwani humo.
Akizungumza
mara baada ya kufanya mazungumzo na wananchi hao wakati alipokuwa anatembelea
mitaa mbalimbali ya Soko Kuu la mjini Chake Chake, Pemba aliwataka wananchi hao
waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato kama kawaida na hakuna mtu
atakayewabughudhi kwani ulinzi umeimarishwa, na waachane na uzushi wa kutokea
vurugu unaoenezwa visiwani humo.
Waziri
Kitwanga alianza matembezi hayo mitaani mara baada ya kufanya mazungumzo na
Kamati ya Ulinzi na Usalama mjini Chake Chake ambapo walimuhakikishia kuwa,
Pemba yote ni salama na ulinzi umeimarishwa na hakuna atakaye fanyiwa vurugu
kwa mtu yeyote atakayefuata sheria.
Waziri
Kitwanga aliwataka wananchi hao kuondoa hofu wanapowaona askari mbalimbali
wakipita mitaani kwani wapo kwa ajili ya kuwalinda wananchi hao pamoja na mali
zao katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka
huu.
“Musiwaogope
askari, na wala msiwe na wasiwasi, mnapowaona shangilieni kwani askari ndio
msaada wako kwa ajili ya usalama wako endapo inapotokea vurugu ya aina yoyote,
mtaenda kupiga kura salama na mtarudi salama, hakuna mtu wa kuwabughudhi,
msitishwe na mtu yeyote,” alisema Waziri Kitwanga na kufafanua;
“Leo
nazunguka mitaa mbalimbali ya hapa Pemba, lengo ni kuchukua maoni yenu pamoja na kuwaondolea
hofu wananchi na kuwahakikishia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimejipanga
vizuri kwa ajili ya kulinda usalama, hivyo jitokezeni kwa wingi siku ya
uchaguzi mkapigie kura kiongozi mnaemtaka.”
Hata
hivyo, Waziri Kitwanga alifanya ziara Mkoa wa Kaskazini Pemba katika msitu wa
Ngezi unaodaiwa kuwa kuna baadhi ya wakimbizi wamejificha katika msitu huo ili
kuokoa maisha yao baada ya kudaiwa kuwa kutatokea na vurugu.
Kitwanga
akiongozana na Wakuu wa Mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba pamoja na
maafisa wa Jeshi la Polisi Pemba, walienda katika msitu huo na kuukagua na
hawakukutana na mtu hata mmoja aliyejificha msituni humo kama inavyodaiwa na
kusambazwa habari na baadhi ya watu wasioitakia mema Zanzibar.
“Ndugu
waandishi wa habari, tumezunguka kwa pamoja kuungalia msitu huu, kuwatafuta hao
wakimbizi, hatujamuona mtu yeyote, ukisikia propaganda ndio hii, watu
hawaitakii mema Zanzibar na Tanzania kiujumla, mmeona kuwa habari hii ni ya
uongo, hakuna mkimbizi yeyote katika msitu huu kama tulivyoshuhudia wote kwa
ujumla,” alisema Kiwanga.
Aliongeza
kuwa, baadhi ya wananchi ambao wana mipango yao binafsi wanawatia hofu wananchi
kwa kutunga habari za uongo kuwa Zanzibar imechafuka, wakati habari hizo hazina
uhalisia wowote.
Hata
hivyo, wananchi wa Pemba walimuhakikishia Waziri Kitwanga wanafanya shughuli
zao za kuwapatia kipato kama kawaida na pia siku ya uchaguzi wataenda kupiga
kura kama kawaida kwani wanaamini amani itakuwepo kama ilivyokuwa sasa.
Waziri
Kitwanga alifanya ziara Zanzibar katika Kisiwa cha Unguja na kuzungumza na
Maafisa wa Jeshi la Polisi na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, na baadae
kumalizia ziara yake kwa kutembelea katika mikoa yote ya Pemba ikiwa ni hatua
ya kuangalia hali ya usalama visiwani humo katika kipindi hiki cha uchaguzi
mkuu katika maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment