WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Sunday 16 July 2017

MASAUNI, MKUU WA WILAYA MUHEZA WAFANYA OPARESHENI USIKU KUWASAKA WAHALIFU MSITU WA AMANI MKOANI TANGA



Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (aliyevaa Kaunda suti), akiongozwa na Afisa Tarafa ya Amani, wilayani Muheza, Ayubu Mhina kumuonyesha eneo la Kihara ambalo ni chanzo cha maji cha Mto Zigi ambalo linasambaza maji sehemu kubwa ya Jiji la Tanga ambalo limeharibiwa na wahalifu kwa kuchimba mashimo wakidai kuwa wanatafuta madini ya dhahabu. Hata hivyo, Jeshi la Polisi linafanya oparesheni katika eneo hilo mara kwa mara na pia linatarajia kujenga Kituo cha Polisi katika eneo hilo ili kupambana na wahalifu hao. Kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Muheza, Oscar Joshua, na kulia ni Mshauri wa Wagambo wilayani humo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akimsikiliza Mhifadhi Msaidizi Hifadhi ya Asili Amani, wilayani Muheza, Bob Matunda (wapili kushoto), alipokua anamuonyesha eneo la Kihara ambalo ni chanzo cha maji cha Mto Zigi lililoharibiwa na wahalifu kwa kuchimba mashimbo wakidai wanatafuta madini ya dhahabu katika eneo hilo. Masauni aliongozana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya muda wa usiku kwenda kuangalia waharibifu hao walivyoliharibu eneo hilo. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akimfafanulia jambo Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo (kulia), mara baada ya kuangalia eneo la chanzo cha maji katika hifadhi ya Msitu wa Asili wa Amani ambalo liliharibiwa na wahalifu kwa kuchimba mashimo katika eneo la Kihara ambalo ni chanzo cha maji, wakidai wanatafuta madini ya dhahabu katika eneo hilo.  Masauni akiongozana na Mkuu wa Wilaya hiyo, walifika eneo hilo la tukio muda wa usiku.  Katikati ni Afisa Tarafa ya Amani, wilayani Muheza, Ayubu Mhina.
Mbunge wa Jimbo Muheza, Balozi Adadi Rajabu akimuonyesha  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), ameneo mbalimbali yaliyoathiriwa na wachimbaji wa madini katika eneo hilo ambalo ni muhimu kutokana kuwa na chanzo cha maji ambayo yanatumika katika eneo kubwa mkoani Tanga. Wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mwanaasha Tumbo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mkoani Tanga kufanya operesheni ya kuwasaka waharibifu  wa chanzo cha maji cha Mto Zigi ambao unapeleka maji Tanga mjini.

Masauni alifika katika eneo hilo la tukio saa mbili usiku na kujionea maeneo yaliyoharibiwa kwa kuchimbwa mashimo makubwa na wahalifu hao wakidai kuwa wanatafuta madini ya dhahabu. Hata hivyo, hakuna mhalifu aliekamatwa katika eneo hilo wakati wa oparesheni hiyo.

Akizungumza katika eneo hilo lililopo Tarafa ya Amani, wilayani humo jana, Masauni ambaye pia aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Muheza, Balozi Adadi Rajabu, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya oparesheni katika eneo hilo usiku na mchana kwa kushirikiana na walinzi wa msitu  ili kuwaondoa wahalifu hao haraka iwezekanavyo.

Masauni alisema licha ya Polisi kuendelea kufanya doria katika eneo hilo lakini wanatarajia kufungua kituo cha polisi ili kuongeza ulinzi zaidi katika eneo hilo muhimu ambalo ndio chanzo cha maji kwa sehemu kubwa ya wakazi wa Mji wa Tanga.

“Tumepanga kuimarisha ulinzi zaidi katika eneo hili kwa kujenga kituo cha polisi ambapo askari wetu watashirikiana na walinzi wa misitu kufanya doria ya kupambana na wahalifu,” alisema Masauni na kuongeza;

“Kwa habari zisizo rasmi tulizozipata katika vyanzo vyetu, hawa wahalifu wanamtandao mkubwa wakishirikiana na watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na hata baadhi ya watumishi wa umma, tutaendelea kufanya uchunguzi huu kwa kina kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya ili kuwabaini wahalifu wote haraka iwezekanavyo.”

Hata hivyo, Masauni alifafanua kuwa, watafanya uchunguzi wa kina kuwachunguza wale wote waliohusika kuwaficha wahalifu iwe askari polisi, iwe mamlaka yoyote nyingine, iwe hakimu au watu wa aina yoyote watachunguzwa. Watanzania tunapaswa tulinde rasilimali za Taifa pamoja na kusimamia ipasavyo.


Masauni alitarajia kwenda mkoani Kilimanjaro kuendelea na ziara yake lakini mara baada ya kupewa taarifa kuhusu uharibifu mkubwa unaofanywa na wahalifu katika msitu huo wa asili, ndipo akaelekeza safari ya kwenda eneo hilo kwanza kuangalia hali halisi pamoja na kuwasaka wahalifu hao ambao inasemekana wana watu hao wanapoona msafara unakuja katika eneo hilo, wanaambizana na utoweka haraka katika eneo hilo.

Katika ziara yake ya siku moja mkoani humo, kwa kutembelea mjini Tanga, Wilaya ya Pangani na baadaye akamalizia Wilaya ya Muheza, Masauni alitoa maelekezo mbalimbali kwa Taasisi zilizochini ya Wizara yake hasa  Jeshi la Polisi na Uhamiaji kuakikisha wanaongeza nguvu kubwa ya kuchunguza na kuzidi kuwasaka wahamiaji haramu mkoani humo, na pia aliamuru ujenzi wa Gereza la Muheza kuanza mara moja ili kupunguza msongamano mkubwa uliopo katika Gereza Kuu la Tanga pamoja na mengineyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Muheza,  Mhandisi Mwanaasha Tumbo alimshukuru Naibu Waziri huyo kwa kufanya ziara katika wilaya yake, na pia alishukuru kwa kuamuru ujenzi wa Gereza Muheza kuanza mara moja na kuahidi kuyafanyia kazi zaidi maelekezo mbalimbali aliyoyatoa wilayani humo.

Hata hivyo, Mhifadhi Msaidizi wa Hifadhi hiyo ya Asili, Bob Matunda alisema mara kwa mara wanawakamata wahalifu hao na kuwafikisha katika vyombo vya usalama, na akaahidi kuwa wataendelea kushirikiana kikamilifu na Jeshi la Polisi katika oparesheni mbalimbali za kuwaondoa wahalifu hao katika eneo hilo.

2 comments:

  1. Anonymous11:11 am

    mbona hamna ukurasa wa kutuma malalamiko ya utendaji wa watumishi wenu ?kwenye website yenu au chombo chochote mlichonacho?

    muwe wawazi na kutupa nafasi hiyo muelewe kilichopo mitaani
    inakera sana

    ReplyDelete
  2. Dear Sir,
    I’m Claiming four subject works and already signed to the settlement agreement with the Garden City Group, Inc and won a awards of let racy in an electronic data base copyright litigation awards of US$ 12.41 in 2018.
    I’m current as active member of Young African Leadership Initiative Network (YALI Network) engaged in Leadership to foster and transforming sustainability of Economic, Security, Human Rights and Good Governance in Tanzania.
    Also, I’m a member of National Peace Corps Association and as well as Member of Alumni Exchange Programs Network working under US Department of State based here in Dar es Salaam, Tanzania.
    Please, May I ask your office to send me a direct deposit payment of US$ 10, 000 to my bank account number: 0152462811800 located at the CRDB Bank PLC MbeziLuis Branch, if your office appreciated my participated and facilitated regarding my helpful informative report provided at the US Investigators Department in order to arrest the Master – Minded of US Embassy bombing attack in Dar es Salaam August 7TH, 1998 in Tanzania.
    I need to get answers if my report was able to help US Investigators and when can I expect to receive a $ 10,000.00 gift?
    Please, I need to be heard and that note I was not sent by any person or institution to come and report, So I am not in the Government body in demanding payment from US Embassy in Tanzania because the US Government promised to pay if I pass the investigation
    I do not need representation, If you think it is right to pay me, do so as soon as possible, without leaking this information to the media in Tanzania.

    Hope to hear from you soon.
    Thank you for your consideration.
    Best Regards,

    JORDAN ERNEST NYEMBE

    MY POSTAL BOX 23453, DAR ES SALAAM, TANZANIA
    MY EMAIL ADDRESS: jordan.nyembe@gmail.com
    MY MOBILE PHONE NUMBERS: +255714908920 Or +255764546826

    ReplyDelete