Na
Felix Mwagara, Nachingwea
WAZIRI wa Mambo ya
Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Mathias Chikawe
ametangaza rasmi kuwa atagombea tena katika nafasi ya ubunge kupitia CCM katika
uchaguzi Mkuu ujao na kulitetea jimbo lake.
Alisema hayo juzi
alipokuwa akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa CCM wa Wilaya na Kata ya
Mtua katika sherehe ya kuwapokea viongozi na wanachama wapya wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliojiunga na CCM wilayani humo.
Chikawe alisema
wananchi wake bado wanamuhitaji kwa hiyo hawezi kuacha kugombea nafasi hiyo
kwani wazee na wananchi mbalimbali katika Kata zote alizokuwa akipita kufanya
mazungumzo nao wanamuomba agombee tena nafasi hiyo.
“Ninyi wenyewe
mashahidi mmewasikia viongozi pamoja na wananchi wanavyosema kuwa bado
wananihitaji kwa hiyo siwezi kuacha wakiwa bado wana mapenzi na mimi kiongozi
wao,” alisema Chikawe na kufafanua kuwa;
“Muda ukifika
nitachukua fomu ya kugombea ili niendelea kuliletea maendeleo makubwa jimbo
letu ambalo mpaka sasa lina mabadiliko makubwa tangu nilipoanza kuliongoza mwaka
2005, ninyi wote ni mashahidi na mmeona mabadiliko hayo ndiyo maana mmefikia
hatua ya kuniomba niendelee kuliongoza jimbo hili.”
Chikawe alisema wakati
akiingia ubunge jimboni humo kulikuwa na hakuna lami na barabara nyingi za
kwenda vijijini zilikuwa hazipitiki na pia maji yalikuwa shida lakini sasa
barabara za lami mjini Nachingwea zimejengwa, maji yanapatikana tena yasio na
chumvi, barabara vijijini zinapitika kwa kuwa zimechongwa vizuri kwa kuwawezesha
wakulima kupitisha mazao yao.
“Sitaweza kuwadharau
ndugu wananchi na pamoja na viongozi wenzangu wa CCM Nachingwea, nimekubali
kugombea tena nafasi hii ya ubunge na kuwaahidi wilaya yetu kuwa na mabadiliko
makubwa zaidi,” alisema Chikawe huku akishangiliwa na mamia ya wananchi
waliofurika katika sherehe hiyo ya CCM.
Wakati huohuo, Waziri Chikawe
alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Regina Chonjo, mabati 2,000 kwa ajili
ya ujenzi wa maabara katika shule 20 za Sekondari za Kata jimboni humo.
Aidha, katika sherehe
hiyo, Chikawe aliwapokea wanachama 23 wa CHADEMA kujiunga na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambapo wanachama hao walirudisha kadi zao na kupewa kadi za CCM
pamoja na kuvalishwa sare za chama hizo.
Kati ya wananchama hao,
pia kulikuwa na viongozi wa Chadema Wilaya ambao ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Wilaya ya
Nachingwea, ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa akina Mama wa Chadema wilayani
humo, Manufreda Malenga pamoja na Katibu wa Siasa Kata ya Mtua, Habibu Oswadi.
Mwisho/-
No comments:
Post a Comment