WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Tuesday 14 April 2015

VIDOKEZO VYA HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. MATHIAS CHIKAWE ALIPOZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI LEO 14 APRILI 2015 JIJINI DAR ES SALAAM KUHUSU MUSTAKABALI WA NCHI KUELEKEA ZOEZI LA KURA YA MAONI YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA NA UCHAGUZI MKUU UJAO



Kwamba Tanzania inaelekea katika matukio makubwa muhimu ya Upigaji Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu.

Uzoefu unaonyesha kuwa wakati kama huu, matukio ya kuashiria uvunjifu wa utulivu na usalama nchini hutokea.

Huko Visiwani Zanzibar, tayari zimetolewa taarifa kuhusu matukio ya uchomaji wa baadhi ya Ofisi ya Vyama vya Kisiasa na kuna taarifa za kuvamiwa wafuasi wa chama mojawapo ya vyama vya kisiasa Visiwani humo wakati wakitokea katika mkutano wa chama chao.

Aidha kuna dalili za baadhi ya Vyama vya Kijamii na Taasisi za Dini kuacha shughuli zao za kikatiba na kuingilia masuala ya kisiasa, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria iliyosajili Vyama na Taasisi hizo.

Wananchi na Viongozi wanashauriwa kutekeleza majukumu yao ya kijamii na kisiasa kwa uhuru bila kushawishi au kushawishiwa na kikundi au mtu yeyote.

Serikali inatoa tahadhari kwa mtu yeyote, kikundi, Chama cha Kijamii, Taasisi ya Dini, au Chama cha Kisiasa kitakachokiuka sheria za utendaji wa shughuli zake na kuhatarisha amani na usalama wa raia na mali zao kuwa kitachukuliwa hatua za kisheria.

Ushauri umetolewa pia kwa Vyama vya Siasa kuepuka kuanzisha misafara wakati wa kuandaa mikutano yake ili kuepuka migongano baina ya wanachama wa vyama hasimu na pia kuwapunguzia askari mzigo wa shughuli za ulinzi.

Kwa upande mwingine, Serikali imechukua tahadhari zote kuhusu matishio ya vitendo vya ugaidi na itashirikiana na Serikali ya Kenya kuhusiana na Watanzania wawili waliokamatwa nchini Kenya kwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi.

Kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina taarifa za wageni wote walioingia nchini kihalali na kwa njia nyinginezo na kwamba zoezi la kuwabaini raia wa kigeni wanaoingia nchini kinyemela linaendelea.

Kwamba kuanzia tarehe 20 Aprili, 2015 Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaanza zoezi la kuvifuta katika Daftari la Msajili Vyama vyote vya Kijamii na Taasisi za Dini zilizosajiliwa chini ya Sheria ya Vyama, Sura 337 ambavyo haviwasilishi Taarifa zao za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada za mwaka kama sheria inavyotaka.  Zoezi hili litaanza na Mkoa wa Dar es Salaam na litaendelea nchi nzima.  Majina ya Vyama na Taasisi zitakazofutwa yatawekwa katika Tovuti ya Wizara www.moha.go.tz na havitaruhusiwa kuendelea na shughuli zake.




No comments:

Post a Comment