Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi
Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Polisi mkoani Manyara kufungua Kituo cha
Polisi katika Makazi ya Kabila la Wahazabe wanaoishi katika Bonde la Yueda
Chini, wilayani Mbulu.
Masauni alisema hayo jana wakati
akizungumza na mamia ya wananchi wa kabila
hilo mara baada ya kukagua jengo la mifugo katika eneo la bonde hilo
ambalo jamii hiyo ilijitenga kwa kuweka makazi pembezoni mwa Mji wa Mbulu.
“Hivi karibuni Kituo cha Polisi
kitafunguliwa hapa ili kulinda usalama wenu katika eneo hili ambalo lilikua
halina kituo cha Polisi kwa miaka mingi. Serikali ya Rais Magufuli ni sikivu
ndio mana nimekuja hapa kuwasikiliza matatizo yenu na kuwatekelezea.” Alisema
Masauni huku akishangiliwa na wananchi hao.
Aliongeza kuwa, mchakato wa kujenga
kituo hicho umeanza na tayari ametoa maelekezo kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi
wa Mkoa huo, kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu,
Wabunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini na Mbulu Mjini.
Pia aliongeza kuwa, uhalifu katika eneo
hilo sasa umepata tiba kwa maana Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi
watahakikisha hali ya usalama unaimarishwa zaidi katika eneo hilo ambalo lipo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbulu
Vijijini, Flatei Massay alisema wananchi wa jimbo lake wanavamiwa, wanaporwa
mali zao ikiwemo mifugo, wanajeruhiwa na wanaingizwa katika umaskini zaidi
kutokana na waalifu kuwa wengi kutokana na ukosefu wa Kituo cha Polisi.
“Nilimuomba na nilimsumbua sana Naibu
Waziri kule Bungeni ili aweze kufika katika eneo hili, ninamshukuru sana kwa
kufika na kutoa maelekezo ya kufunguliwa kituo cha polisi, sasa wakazi wa eneo
hili tunatarajia kupata ulinzi wa kutosha baada ya kituo hicho kufunguliwa hivi
karibuni,”alisema Massay.
Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani humo,
Francis Massawe alisema amepokea maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri na mchakato
utaanza rasmi na hatimaye kituo cha Polisi kitakuwepo katika eneo hilo na
wananchi wataendelea na shughuli zako za kutafuta mahitaji yao kwa usalama
zaidi.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
No comments:
Post a Comment