JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU
ZOEZI LA USAILI WA NAFASI YA MKAGUZI MSAIDIZI WA UHAMIAJI LILILOFANYWA NA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KATIKA UWANJA MPYA WA TAIFA TAREHE 13 JUNI,
2014
Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi imebaini taarifa mbalimbali zinazozungumzwa na ambazo zimetolewa katika
baadhi ya vyombo vya habari kuhusu zoezi
la usaili wa nafasi ya Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji lililofanywa na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi tarehe 13 katika Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam.
Wizara ingependa kutoa
ufafanuzi kuhusu baadhi ya tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wadau kama
ifuatavyo:
1. RUSHWA
Tuhuma
za rushwa zinazoambatanishwa na zoezi hili ni hisia tu za wahusika kwani,
kwanza hazina ushahidi, na pia usaili ulifanywa kufuatana na kanuni na sheria zinazosimamia
ajira za watumishi wa Umma.
2. ULINZI
Katika
Uwanja wa Taifa kulikuwa na Maafisa mbalimbali toka Taasisi za Wizara ya Mambo
ya Ndani ya nchi ambao walikuwepo kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa
usalama.
3. WINGI WA WASAILIWA
Nafasi
za Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji zilitangazwa katika magazeti na Tovuti ya
Wizara na Idara ya Uhamiaji kufuatana na taratibu Serikali zinazosimamia
ujazaji wa nafasi za kazi katika utumishi wa umma kwa lengo la kuiweka wazi kwa
umma wa Watanzania na matokeo yake wahitimu zaidi ya 20,000 walitumia haki yao
ya msingi kuomba nafasi hizo.
Kufuatana
na wingi wa waombaji, Wizara ilifanya zoezi la mchujo wa awali ambao hatimaye ulibakiza
kiasi cha maombi 10,000 yenye waombaji wenye sifa zinazohitajika.
Aidha
kutokana na wingi huo, na haki ya kila muombaji ya kupatiwa nafasi ya
kushindania nafasi hizo, ilibidi Wizara ifanye utaratibu wa kutafuta eneo lenye
nafasi ya kutosha ya kuweza kuwapokea wasailiwa, ambalo hatimaye ilionekana iwe
Uwanja mpya wa Taifa.
Wingi
wa wasailiwa ni matokeo ya kidemokrasia ya kutoa nafasi kwa kila raia
kushindania nafasi za ajira zinazotolewa nchini ili mradi awe na sifa.
4. BAADHI YA WASAILIWA KUTOKUWA NA KALAMU
Maandalizi
ya usaili ni pamoja na kuwa na vifaa vya kawaida vya kushiriki usaili hivyo
msailiwa aliyefika katika eneo la usaili akiwa mikono mitupu ni yule ambaye
hakujiandaa, wala kuwa na kalamu haihitaji kutangaziwa.
5. UFINYU WA ENEO
Uwanja
mpya wa Taifa Dar es Salaam una uwezo wa kukaliwa na watu 60,000 hivyo idadi ya
wasailiwa 10,000 waliokuwapo uwanjani hapo haikuwa tishio kwa usalama wao.
MWISHO
Nia ya
Wizara haikuwa kuleta usumbufu kwa mtu yeyote ila kutoa nafasi sawa kwa
walioleta maombi kushindania nafasi zilizotangazwa.
Imetolewa na:
Sgn
Isaac J. Nantanga
MSEMAJI
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
14
JUNI, 2014
No comments:
Post a Comment