Jeshi la Magereza litafanya
Maadhimisho ya Siku ya Magereza Nchini tarehe 20 Juni, 2014 kuanzia saa 2:00
asubuhi katika Viwanja vya Chuo cha Maafisa wa Magereza Ukonga, Dar es Salaam
ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe.
Mathias Chikawe(MB).
Kwa mujibu wa taarifa rasmi
iliyotolewa leo Juni 18, 2014 na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John
Casmir Minja Maadhimisho haya ni ya pili kufanyika tangu Jeshi la Magereza
Tanzania lianzishwe rasmi mwaka 1931. Madhumuni ya Siku ya Magereza ni:-
- Kuelimisha jamii juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Magereza katika utekelezaji wa majukumu yake ya uhifadhi na Urekebishaji wa wahalifu kupitia shughuli za viwanda Vidogo Vidogo, Ujenzi, Kilimo, Ufugaji na Ufundi katika fani mbalimbali.
- Kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika suala zima la Urekebishaji wa wahalifu na;
- Kutoa elimu kwa umma juu ya huduma na taratibu za Uendeshaji wa Magereza Nchini.
Shughuli zitakazofanyika siku
hiyo ni pamoja na ufunguzi wa Duka la Bidhaa zisizolipiwa Kodi (Duty Free Shop)
Gereza Keko, kukagua shughuli zinazofanyika kwenye Ofisi za Chama cha Ushirika
wa Kuweka na Kukopa kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza (TPS SACCOS) eneo la
Keko, kufungua Karakana ya Uhunzi Gereza Ukonga, Gwaride Maalum, Onesho kutoka
Kikosi Maalum la utayari wa Kutuliza Ghasia Magerezani. Ushuhuda wa Mfungwa
aliyepata Shahada ya Sheria (LLB) akiwa gerezani, Burudani Maalum ya
muziki kutoka kwa wafungwa, askari wa kike waliohitimu mafunzo maalum
kukabidhiwa vyeti na Mgeni rasmi na maonesho ya kazi mbalimbali zinazofanywa na
Jeshi la Magereza.
Vyombo vya Habari na Wananchi
wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mikoa jirani wanakaribishwa kuja kushiriki
katika Maadhimisho haya ili wapate nafasi ya kuona na kujifunzia shughuli
mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Magereza.
Imetolewa na;
Lucas Ambrose Mboje, Mkaguzi wa Magereza,
Afisa Habari Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
18 Juni, 2014,
DAR ES SALAAM.
Lucas Ambrose Mboje, Mkaguzi wa Magereza,
Afisa Habari Makao Makuu ya Jeshi la Magereza,
18 Juni, 2014,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment