JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
SIKU YA
WAKIMBIZI DUNIANI KUADHIMISHWA
TAREHE 20
JUNI, 2014
Tarehe 20 Juni ya
kila mwaka ni siku ya Wakimbizi duniani na kwa Tanzania siku hiyo itaadhimishwa kitaifa hapa Dar es
Salaam katika Hotel ya Sea Cliff, ambapo mgeni rasmi katika halfa hiyo atakuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe.
Kufuatana na Shirika
la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kauli mbiu ya maadhimisho
ya mwaka huu ni “Familia moja kusambaratika na vita ni wengi mno” au kwa
Kiingereza “1 family torn apart by war is too many”.
Taarifa hiyo
inaongeza kuwa kiasi cha watu 43 milioni duniani kote wamelazimika kuyahama
makazi yao kwa sababu ya vita, machafuko au majanga ya asili, na kati yao kiasi
cha milioni 10 wanahudumiwa na Shirika hilo.
Kwa upande wa
Tanzania, kiasi cha wakimbizi wapya wanaoomba hifadhi imepungua ilikinganishwa
na miaka ya nyuma ambapo kuna wakati idadi yao ilikaribia kufikia milioni
moja. Kupungua huku ni ishara ya kuimarika
kwa hali ya usalama ndani ya nchi walizotoka wakimbizi hao, hususan nchi za
eneo la Maziwa Makuu. Hata hivyo, bado
hali si shwari sana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hali
inayosababisha baadhi ya raia wa nchi hiyo kuikimbia na kwenda kuomba hifadhi
ya ukimbizi katika nchi nyingine ikiwemo Tanzania.
Mfano wa mafanikio
yaliyopatikana hapa nchini kuhusiana na suala la Wakimbizi ni kufungwa kwa
kambi za wakimbizi zaidi ya kumi na mbili ambapo kambi ya mwisho kufungwa ya
Mtabila iliyokuwa wilayani Kasulu mkoani Kigoma iliyokuwa na raia zaidi ya
35,000 toka Burundi ilifungwa mwishoni mwa Desemba, 2012. Sasa hivi Tanzania imebakiwa na kambi moja tu
ya Nyarugusu, wilayani Kasulu mkoani Kigoma ambayo ina wakimbizi takribani
65,084, wengi wao wakiwa ni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi na Jumuiya ya Kimataifa linaamini suluhisho la
kudumu kwa tatizo la wakimbizi ni kwa wakimbizi kupata nafasi ya kurejea kwao
kwa hiari, mara baada ya mazingira yaliyowafanya kuzikimbia nchi zao
kutoweka. Jambo hili litafanyika na
kufanikiwa pale Serikali za nchi na Jumuiya ya Kimataifa zitakapochukua hatua
za makusudi kuhakikisha kuwa sababu zinazowafanya raia wa nchi mbalimbali
kuzikimbia nchi zao zinatafutiwa ufumbuzi.
Hii ni pamoja na kuwa na Serikali zinazozingatia sheria, utawala bora na
haki za binadamu.
Imendaliwa
na: Isaac J. Nantanga – Msemaji wa
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
19 Juni, 2014
No comments:
Post a Comment