Na Felix Mwagara
SERIKALI imewapa uraia
wa Tanzania Wakimbizi wa Kisomali wenye asili ya Kibantu 1,514 waliokuwa
wanaishi katika Makazi ya Chogo, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Wakimbizi hao ambao
walikimbia nchi yao Somalia baada ya vita kutokea mwaka 1990 ambapo baadhi yao
3,000 walikimbilia nchini kwa kutambua kuwa ndipo mababu zao walikotoka,
Serikali iliwapokea na kuwahifadhi katika Kambi ya Mkuyu iliyopo Mkoani Tanga
ambapo walikuwa wakipata msaada kutoka Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani
(UNHCR).
Akizungumza jana baada
ya kuwapa vyeti vya uraia wakimbizi hao ambao kwasasa ni raia halali wa
Tanzania, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema wakimbizi
hao walihamishwa na Serikali mwaka 2003 kutoka Kambi ya Mkuyu kuja katika
Makazi ya Chogo ili wapatiwe mashamba kwa ajili ya kujishughulisha na kilimo
ili waweze kujitegemea.
“Nachukua nafasi hii
kuwapongeza wote waliopewa uraia wa Tanzania, wajisikie kuwa wao ni raia huru
sawa na Watanzania wengine. Hata hivyo nawasihi muwe waadilifu na watiifu kwa
sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Chikawe.
Chikawe pia alitoa
pongezi kwa UNHCR kwa kujenga miundombinu muhimu katika makazi hayo ya Chogo na
pia kuwawezesha wakimbizi hao kuishi maisha ya kujitegemea wenyewe kabla hata
ya kuwa raia.
Hata hivyo, Waziri
Chikawe aliwataka wakimbizi 150 katika makazi hayo ya Chogo ambao hawakuomba kuwa
raia wa Tanzania kwa nia ya kurudi nchini Somalia pale hali ya amani
itakapopatikana wanapaswa kuendelea kutii sheria za nchi zinazotawala hifadhi
ya ukimbizi nchini.
Aidha, Mwakilishi Mkazi
wa UNHCR, Joyce Mends-Cole katika hafla hiyo aliishukuru Serikali ya Tanzania
kwa kuwapa uraia wakimbizi hao na Shirika lake litaendelea kutoa misaada
mbalimbali kwa wakimbizi waliobaki katika makazi hayo pamoja na sehemu nyingine
nchini.
Hafla hiyo ya ugawaji
wa vyeti vya uraia ilihudhuriwa na Maofisa wa Idara ya Wakimbizi na Uhamiaji
zilizopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwakilishi wa Mkuuu wa Mkoa wa Tanga
na Serikali ya Kijiji cha Chogo pamoja na Maofisa wa UNHCR.
Mwisho/-
No comments:
Post a Comment