Felix
Mwagara, Nachingwea
WAZIRI wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Mathias Chikawe ametoa
msaada wa mabati 100 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Kata ya Nditi pamoja na jezi za mpira wa miguu kwa timu sita zilizopo
katika kata hiyo, jimboni kwake Nachingwea mkoani Lindi jana.
Waziri Chikawe pia
ametoa mifuko 15 ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti uliopo katika Kata
hiyo pamoja na kuwataka wananchi washirikiane kufanya kazi ili kuiletea
maendeleo kata yao ambayo ni moja ya kata ni muhimu katika Jimbo lake la
Nachingwea.
Akizungumza baada ya
kutoa msaada huo pamoja na kusikiliza kero mbalimbali za viongozi wa Kata ya Nditi
katika mkutano na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Kata hiyo, Wajumbe wa
Mabaraza wa Jumuiya zote za CCM Kata, Viongozi wa Dini na Wajumbe wa Baraza la
Wazee wa Kata alisema chama chake CCM kipo bega kwa nega na wananchi ikiwa na
lengo la kuwaletea maendeleo zaidi.
“Nafurahi leo (jana)
kuzungumza na viongozi wa Kata hii, nimekuja hapa kusikiliza kero zenu ambazo
mnazijua ndani ya kata hii, hata hivyo nimezisikiliza kupitia hotuba yenu
pamoja na maswali mbalimbali mlioniuliza, na tayari baadhi ya maswali yenu
nimeyajibu na mlichokuwa mnahitaji nimewasaidia,” alisema Chikawe.
Chikawe aliongeza kuwa,
licha ya kuendelea kutoa misaada ya kijamii mbalimbali katika jimbo lake lakini
pia amepanga kukuza michezo katika jimbo hilo ambapo ameanza kwa kutoa msaada
wa jezi kwa timu sita za mpira wa miguu katika Kata ya Nditi na baadaye
atahamia katika kata zingine za jimboni kwake.
“Michezo ni muhimu kwa
afya na pia muhimu kwashughulisha vijana hawa, maana kuna msemo usemao
‘Usipowashughulisha vijana hawa watakuja kukushughulisha, sasa ngoja
tuwashughulishe kabla ya kutushughulisha,” alisema Chikawe.
Akizungumza baada ya
kupokea msaada wa jezi za mpira wa miguu, Afisa Mtendaji wa Kata ya Nditi,
Patrick Mwasambungu alimshukuru Waziri Chikawe kwa msaada huo na jezi hizo
atazigawa kwa timu hizo katika kata yake.
Aidha, Chikawe
aliwataka viongozi hao kutoa elimu zaidi kwa wananchi wao endapo rasimu ya pili
ya Katiba ikipitishwa na Bunge la Maalum la Katiba washiriki kikamilifu katika
kupiga kura ya maoni kwani Katiba ndio msingi wa maisha ya kila Mtanzania na
muelekeo wa nchi yetu.
Waziri Chikawe yupo
jimboni kwake Nachingwea kwa ziara maalum ya kuzungumza na viongozi wa CCM
katika kata zake pamoja na kusikiliza kero mbalimbali zinazowasibu katika kata
zao.
Mwisho/-
No comments:
Post a Comment