WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Monday, 15 September 2014

WAZIRI CHIKAWE AWAONYA WAKIMBIZI NYARUGUSU MKOANI KIGOMA


Felix Mwagara
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amewataka  Wakimbizi wa Kambi ya Nyarugusu kuacha mara moja tabia ya kuwaozesha watoto wao wenye umri mdogo kwani tabia hiyo inawaletea matatizo makubwa watoto wao wakati wanapojifungua.
Akizungumza na mamia ya wakimbizi hao katika Ukumbi wa Mikutano  katika kambi hiyo iliyopo wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma, Waziri Chikawe alisema katika maisha yake, yeye ni mpambanaji wa kupinga ndoa za utotoni ambazo zinawaletea madhara makubwa watoto.
Chikawe alifafanua kuwa, tabia hiyo inayofanywa na wakimbizi hao dhidi ya watoto wao inawasababishia watoto hao kupatwa na matatizo makubwa kipindi wanapojifungua kwani viungo vyao vya uzazi havipo tayari kwa ajili ya kuzaa hivyo aliwataka familia za wakimbizi hao kuacha tabia hiyo ya kikatili dhidi ya watoto wao na pia inawakosesha haki zingine za msingi watoto hao.
“Wapeni haki zao watoto wenu, utamaduni huu sio mzuri wa kuwaozesha watoto wadogo, mnatakiwa kuuacha na kuulaani kwani mkifanya hivyo mtakuwa mnawaletea matatizo makubwa watoto wenu hasa wanapojifungua,” alisema Chikawe.
Aidha, Waziri Chikawe aliwataka wakimbizi katika kambi hiyo kuwa makini na ugonjwa wa Ukimwi kwani ugonjwa huo unaendelea kuua maelfu ya watu duniani na pia bado hauna dawa, na kuwataka wakimbizi hao kuacha tabia ya ufuska na endapo watashindwa basi watumia kondomu kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo hatari.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole, aliwaonya wakimbizi hao kuacha tabia hiyo ya kuwaoza watoto wao ambao wapo chini ya miaka 18 kwani kwa kufanya hivyo Wakimbizi hao watashindwa kupata nafasi ya kwenda nchini Marekani.
“Si mnajua tunawaandaa kwenda Marekani?, kama mnalijua hilo basi endapo mkimbizi yeyote akimpa mimba mtoto mdogo basi hataweza kupata nafasi ya kwenda nchini humo, hivyo kuweni makini ili muweze kwenda nchini Marekani,” alisema Joyce.
Zaidi ya wakimbizi 30,000 wa Kambi ya Nyarugusu wanatarajiwa kuhamishiwa katika nchi ya Marekani kuanzia mwaka 2015.
Waziri Chikawe ambaye aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi nchini, Harrison Mseke pamoja na maafisa wengine wa wizara yake, amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Kigoma ambapo katika siku hizo alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma.
Pia alikitembelea Kituo cha Mpito cha Wakimbizi (NMC) kilichopo mjini Kigoma na baadaye akamalizia ziara yake katika Wilaya ya Kasulu mkoani humo kwa kuitembelea Kambi kubwa ya wakimbizi ya Nyarugusu inayowahifadhi wakimbizi zaidi ya 60,000 ambapo wengi wao wakiwa ni kutoka nchini Kongo, Burundi na wachache kutoka  mataifa mengine.


  

No comments:

Post a Comment