Idadi ya raia wa Burundi
wanaoingia nchini kutafuta hifadhi ya ukimbizi inazidi kuongezeka siku hadi
siku ambapo hadi kufikia tarehe `17 Oktoba, 2015 idadi hiyo ilikuwa imefikia
107,112.
Raia hawa wa Burundi
wanaendelea kuingia nchini kupitia vijiji vya mpakani na wengi wao ni wanawake
na watoto kutoka Mkoa wa Makamba nchini Burundi.
Vijiji wanapoingilia raia
hawa kutoka Burundi ni pamoja na Bukililo na Katanga wilayani Kankonko, na
Kitanga, Kigadye, Manyovu, Kilelema, Biharu, Migongo na Herushingo wilayani
Kasulu. Kijiji kingine ni Mabamba
kilichopo wilayani Kibondo, ambapo wengine hupitia wilayani Ngara mkoani
Kagera.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi
(UNHCR) na wadau wengine, imekuwa ikiwahifadhi wakimbizi hawa katika makambi ya
wakimbizi ambapo hupatiwa huduma zote muhimu.
Huduma hizo ni pamoja za malazi, chakula, afya, elimu na ulinzi.
Wakati huo huo, Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi imeanza zoezi la kuwahamisha wakimbizi wa Burundi
waliokuwa wakihifadhiwa kwa muda katika kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu na kuwapeleka
katika kambi ya Nduta iliyoko wilayani Kibondo.
Zoezi hili ambalo limeanza
tarehe 04 Oktoba, 2015 linalenga kupunguza msongamano uliokuwapo katika kambi
ya Nyarugusu ambayo hadi wakati huo ilikuwa na jumla ya wakimbizi 102,773
kutoka nchini Burundi.
Tangu zoezi hili lianze,
kiasi cha wakimbizi 3,808 kutoka nchini Burundi wameshahamishiwa katika kambi
ya Nduta kutoka kambi ya Nyarugusu ambayo inahifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC). Kambi ya Nyarugusu ina
kiasi cha wakimbizi 60,000 kutoka DRC.
Zoezi la kuwahamisha
wakimbizi hawa kutoka nchini Burundi litaendelea hadi wakimbizi wote kutoka nchi
hiyo walioko katika kambi ya Nyarugusu watakapoisha.
Pamoja na kambi ya Nduta,
maeneo mengine yanayoendelea kuandaliwa ili kuwahifadhi wakimbizi hawa kutoka
Burundi ni Mtendeli na Karago yaliyoko wilayani Kakonko mkoani Kigoma.
Aidha, wakimbizi wote
wanaoendelea kuingia nchini kutoka Burundi kwa sasa hupelekwa moja kwa moja
katika kambi ya Nduta badala ya kambi ya Nyarugusu.
No comments:
Post a Comment